Ofisi ya Msajili wa Hazina yafanya kikao cha bajeti na TANAPA

Na Mwandishi wa OMH
Kibaha. Ofisi ya Msajili wa Hazina ilifanya kikao na Wajumbe wa Kamati ya Bajeti ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Alhamisi, Aprili 10, 2025, katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kibaha, mkoani Pwani.
Kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti, Peter Maungo, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Mashirika ya Kibiashara ya Umma kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Kikao hicho kilikuwa na dhima ya kujadili na kupitisha bajeti mpya ya TANAPA kwa mwaka 2025/2026, ambayo kipaumbele chake ni kuongeza fursa za uwekezaji, kuanzisha mazao mapya ya utalii, kuboresha miundombinu ya utalii, kuimarisha ulinzi mkakati kwa kutumia teknolojia, shughuli za uhifadhi na tafiti, pamoja na kuongeza fursa za ajira kwa kuzingatia miongozo ya shirika la ubora wa kimataifa (ISO).
Pia, bajeti hiyo inalenga kudhibiti mimea vamizi na wanyamapori wakali na waharibifu, kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi, na kutekeleza miradi mingine ya maendeleo.
Kamati ya Bajeti ya Shirika iliongozwa na Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Juma Nassoro Kuji, ambapo aliambatana na wataalamu waandamizi kutoka idara mbalimbali za Shirika hilo.
Katika kikao hicho, Kamishna Kuji alieleza kwa kina mwelekeo wa kimkakati wa Shirika katika mwaka wa fedha 2025/2026, akisisitiza umuhimu wa kuongeza ufanisi katika matumizi ya rasilimali, kuimarisha mifumo ya usimamizi, na kukuza ushirikiano kati ya TANAPA na wadau mbalimbali wa uhifadhi na utalii.