Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MSAJILI WA HAZINA

Gawio la serikali kutoka benki ya TADB lapaa kwa 556%
17 Apr, 2025
Gawio la serikali kutoka benki ya TADB lapaa kwa 556%

Na Mwandishi wa OMH

Dar es Salaam. Uwekezaji wa Serikali, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), umeendelea kuonesha matokeo chanya, ambapo kwa mwaka ulioishia Desemba 2024, benki hiyo imeongeza gawio kwa Serikali kwa asilimia 556 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

Gawio hilo lililotangazwa katika Mkutano Mkuu wa mwaka Alhamisi, Aprili 17, 2025, limeongezeka kutoka Sh850 milioni kwa mwaka ulioishia Disemba 2023 hadi kufikia Sh5.583 bilioni kwa mwaka ulioishia Disemba 2024.

Akizungumza jijini Dar es Salaam mara baada ya kupokea gawio hilo, Mwakilishi wa Msajili wa Hazina, Bw. Mohamed Nyasama, alieleza kuwa ongezeko hilo ni uthibitisho wa mafanikio ya uwekezaji wa Serikali katika benki hiyo.

Aidha, Bw. Nyasama aliipongeza Bodi ya Wakurugenzi na Watumishi wa TADB kwa kusimamia vyema utekelezaji wa majukumu ya benki, hali iliyowezesha kuimarika kwa huduma za kifedha kwa wananchi wa Tanzania Bara na Visiwani.

“Hii ni taarifa ya mafanikio ya kusheherekea. Benki imefanya vizuri sana katika vigezo vya kiuwekezaji na kifedha,” alisema Bw. Nyasama, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mipango, Tafiti na Maendeleo-Ofisi ya Msajili wa Hazina, ambayo ndio mwanahisa pekee wa TADB.

Aliongeza kuwa kiwango cha mikopo chechefu kimeshuka kutoka asilimia 3.7 mwaka 2023 hadi asilimia 2.7 mwaka 2024, jambo linaloashiria uimara wa usimamizi wa mikopo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw Frank Nyabundege, alieleza kuwa faida ya benki kabla ya kodi imeongezeka kwa asilimia 31, kutoka Sh18.8 bilioni mwaka 2023 hadi Sh24.7 bilioni mwaka 2024.

Alifafanua kuwa ongezeko hilo limechangiwa na kupanuka kwa utoaji wa mikopo katika minyororo ya thamani ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Bw. Nyabundege alisema jumla ya mikopo iliyotolewa iliongezeka kutoka Sh331 bilioni mwaka 2023 hadi Sh534 bilioni mwaka 2024, ongezeko la zaidi ya asilimia 61.

“Mafanikio haya yametokana kwa kiasi kikubwa na uwezeshaji wa Serikali, hususan katika Awamu ya Sita ya Uongozi wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan.

”Tangu alipoingia madarakani mwaka 2021, Mheshimiwa Rais amekuwa na utashi wa kisiasa wa kuiwezesha TADB ili iwafikie wakulima kwa ufanisi zaidi kwa kutambua kuwa sekta hiyo inaajiri zaidi ya asilimia 67 ya watanzania.”

 Bw. Nyabundege alisema kuwa serikali ilitoa mtaji wa Sh208 bilioni mwaka 2021, na Sh174 bilioni mwaka 2024, kiasi ambacho kimeongeza mtaji wa benki kutoka Sh60 bilioni hadi Sh442 bilioni.

Jambo hili limepelekea kuimarika kwa uwezo wa benki na matokeo yake thamani ya mali kukua kutoka Sh607 bilioni mwaka 2023 hadi Sh917 bilioni mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 51.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi  ya TADB, Bw. Ishmael Kasekwa, alisema kuwa bodi itaendelea kusimamia benki hiyo kwa weledi na kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji.