Msajili Hazina awapa heko Mamlaka ya Usafiri wa Anga

Dodoma. Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu amelipongeza Baraza la Wafanyakazi la Mamlaka ya usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kwa kuwa chachu ya maamuzi yenye tija katika ufanisi wa sekta ya usafiri wa anga nchini.
Bw. Mchechu aliyasema hayo wakati wa mkutano wa pili wa Baraza la Wafanyakazi la TCAA jijini Dodoma na kuongeza kuwa ongezeko la mapato linalotokana na mchango wa sekta ya usafiri wa anga umechangiwa na ufanisi ya mamlaka hiyo kwa kuongeza ushawishi kwa wadau kutoka nchi mbalimbali wanaotumia anga la Tanzania.
“Baraza hili si tu ni jukwaa la mijadala bali ni daraja la kuelekea maboresho ya kweli ya mazingira ya kazi hivyo inapaswa kila mfanyakazi kushiriki safari ya maendeleo ya taasisi hii,” alisema Bw. Mchechu
Bw. Mchechu alisisitiza umuhimu wa vikao vya baraza katika kuimarisha misingi ya demokrasia sehemu za kazi na kuwahamasisha wajumbe kuhakikisha wanawasilisha mrejesho kwa watumishi wenzao waliowawakilisha ili kujenga mshikamano na ufanisi katika kutekeleza majukumu yao.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Bw. Salim Msangi aliahidi kuendeleza maboresha katika mazingira ya kazi ili kila mtumishi atimize wajibu wake kwa weledi na kuisukuma mbele sekta ya usafiri wa anga.
“Ni muhimu kila mtumishi afahamu kuwa TCAA inajengwa kwa juhudi za pamoja na mafanikio yanayoonekana ni matokeo ya ushirikiano, kusaidiana na kutimiza malengo ya serikali kwa kutoa huduma bora kwa Watanzania na wadau wetu kwa malengo makubwa zaidi” alisema Bw. Msangi.