Ofisi ya Msajili Hazina yanunua asilimia 10 hisa za Benki ya Ushirika

Na Mwandishi wa OMH
Dodoma. Serikali, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, imenunua asilimia 10 ya hisa za Benki ya Ushirika Tanzania, iliyoanzishwa kwa lengo la kuondoa changamoto ya mifumo ya fedha kutoelewa soko na tabia za kilimo nchini.
Hisa hizo za benki ambayo ilizinduliwa rasmi Jumatatu, Aprili 28, 2025, na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan, zimenunuliwa kwa Sh5.8 bilioni.
Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu alikabidhi hundi ya kiasi hicho cha fedha kwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya benki hiyo mbele ya Mhe. Rais.
Sanjari na Ofisi ya Msajili wa Hazina, vyama vya Ushirika vinamiliki asilimia 51 ya hisa kwenye benki hiyo, Benki ya CRDB asilimia 20, na wawekezaji binafsi asilimia 19.
Kwasasa benki hiyo ambayo ilianza shughuli zake Oktoba 2024 baada ya kupewa leseni ya muda na Benki Kuu ya Tanzania, ina mtaji wa Sh58 bilioni.