Msajili wa Hazina azindua huduma ya uwekezaji wa hisa kidijitali

Na Mwandishi wa OMH
Dar es Salaam. Msajili wa Hazina Bw. Nehemiah Mchechu amezindua huduma mpya ya uwekezaji wa hisa kupitia Popote Mobile App.
Huduma hii itawawezesha wateja kununua, kuuza na kuangalia mwenendo wa bei za hisa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Huduma hiyo mpya ambayo ni zao la ushirikiano kati ya benki ya TCB na DSE, ilizinduliwa Ijumaa, Februari 21, 2025, jijini Dar es Salaam.
Uzinduzi wa huduma hii unakuja katika wakati ambapo soko la mitaji la Tanzania linahitaji mageuzi ya kidijitali ili kuongeza ushiriki wa wananchi.
Popote Mobile App ni suluhisho la kisasa ambalo linaruhusu Watanzania kufanya miamala ya hisa kupitia simu zao za mkononi, hali itakayochochea ukuaji wa uchumi na kupanua fursa za uwekezaji katika masoko ya mitaji.
Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Mchechu, aliipongeza Benki ya TCB kwa kuendelea kuwa kinara katika teknolojia ya kidijitali na kuleta ubunifu unaokidhi mahitaji ya wateja.
Mchechu aliiagiza benki hiyo kuhakikisha huduma hii inakuwa rahisi, salama na inapatikana kwa wananchi wote bila vikwazo vya kiufundi.
“DSE na TCB mnapaswa kupunguza gharama za uwekezaji na kuongeza ufanisi wa miamala ya hisa kwa kutumia mifumo ya kidijitali,” alisema.
Aliongeza: “Serikali inalenga kuimarisha ushiriki wa wananchi katika masoko ya mitaji na kuchochea maendeleo ya uchumi wa soko huria nchini.”
Mchechu pia aliziagiza DSE na TCB kuhakikisha kwamba watanzania wanapata elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa kuwekeza katika soko la mitaji.
“Ni muhimu kuongeza ushiriki wa wananchi katika uwekezaji wa hisa ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kusaidia sekta binafsi kupata mtaji wa muda mrefu kwa njia endelevu.”
Afisa Mtendaji Mkuu wa TCB, Bw. Adam Mihayo, alieleza kuwa uzinduzi wa Popote Mobile App ni hatua muhimu katika kuimarisha ujumuishaji wa kifedha na kuleta mageuzi katika soko la mitaji nchini.
Aliongeza kuwa kuunganishwa kwa mifumo ya benki na DSE kutapanua wigo wa uwekezaji kwa kurahisisha upatikanaji wa hisa kwa wawekezaji wa rika zote.
“Matokeo yake ni kuvutia wawekezaji wapya katika soko la hisa na hivyo kuongeza ukwasi,” alihitimisha Bw. Mihayo.
Mtendaji Mkuu wa DSE, Bw. Peter Nalitolela, alisema kuwa teknolojia hii itarahisisha ununuzi na uuzaji wa hisa moja kwa moja kupitia simu za mkononi.
“Mtu hatalazimika kutembelea madalali wa hisa au ofisi za soko na hivyo kupanua wigo wa ushiriki wa wananchi katika soko la mitaji na kusaidia kampuni zinazoorodheshwa kupata mtaji,” alisema.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMA), Nicodemus Mkama, alisema uzinduzi wa Popote Mobile App ni hatua muhimu katika kuhakikisha Watanzania wanapata urahisi wa kuwekeza kupitia teknolojia ya kidijitali.
“Teknolojia hii itawawezesha watumiaji kufanya miamala ya hisa kwa njia salama na rahisi, bila vikwazo vya kifedha au kijiografia,” alisema Bw. Mkama.