Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MSAJILI WA HAZINA

Mageuzi tasisi za umma: Njia ya kuongeza ufanisi
02 Nov, 2024
Mageuzi tasisi za umma: Njia ya kuongeza ufanisi

 

Dar es Salaam. Katika zama hizi za maendeleo makubwa ya teknolojia na matarajio ya jamii yanayobadilika mara kwa mara, taasisi za umma zinakabiliwa na shinikizo kubwa la kufanya mageuzi.

 

Katika ulimwengu huu wa sasa, mageuzi haya si hiari; ni lazima ili kuboresha huduma na kuendeleza serikali yenye ufanisi zaidi.

 

Katika safari hii ya mabadiliko, Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) imeibuka mstari wa mbele, ikiongoza mfululizo wa mipango iliyoandaliwa kuboresha utendaji wa taasisi za umma.

 

Kipengele muhimu cha mipango hii ni kutoa uhuru wa kimkakati kwa taasisi za umma ili kuunda mazingira yanayowezesha ubunifu na kuharakisha maamuzi.

 

Lengo kuu la serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ni kuziwezesha taasisi hizi kujiendesha kibiashara ili kupunguza utegemezi wao kwa serikali kuu, na kuongeza mchango wao kwenye Mfuko mkuu wa serikali.

 

Serikali inaamini kwamba kwa kuruhusu taasisi na mashirika ya umma kujiendesha kwa uhuru zaidi, kutawezesha kukidhi mahitaji ya soko kwa ufanisi zaidi.

 

Hivi karibuni, Bw. Nehemiah Mchechu, Msajili wa Hazina, alitangaza kwamba hadi kufikia Agosti 12, mwaka huu, uhuru wa kujiendesha ulikuwa umetolewa kwa taasisi na mashirika ya umma 57.

 

Aidha, Ofisi ya Msajili wa Hazina inaendelea kufuatilia kwa ukaribu taasisi na mashirika ya umma ili kuona  kama zinakidhi/ yanakidhi vigezo vya kupewa uhuru wa kujiendesha.

 

 

Ni shauku ya Bw. Mchechu kuona taasisi na mashirika yote 309, yenye mtaji wa uwekezaji wa Sh86 trilioni hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu, yanaendesha shughuli zao kwa ufanisi.

 

Hivi sasa, ni taasisi 91 pekee zinazofanya kazi kibiashara.

 

Hali hii inatia wasiwasi kwani mwisho wa siku ni serikali ndio inatwishwa mzigo wa kuziendesha taasisi na mashirika hayo kwa kuyapatia ruzuku ambazo zingeweza kutumika kwaajili ya huduma za kijamii na ujenzi wa miundombinu.

 

Hali hii inaonyesha hitaji la mageuzi, labda kupitia upya muundo, au kutumia mbinu za soko ili kuboresha utendaji.

 

Hata hivyo, mabadiliko yoyote yanapaswa kuzingatia maslahi ya umma na uendelevu wa kiuchumi ili kuhakikisha malengo ya taasisi na mashirika ya umma  yanalingana na malengo makubwa ya serikali.

 

Kwa upande mwingine, kati ya kampuni 91 zinazojiendesha kibiashara, ni 35 pekee ambazo serikali ina hisa nyingi.

 

Tafsiri yake ni kuwa serikali ina hisa chache kwenye kampuni 56.

 

 

Hizi data zinaashiria kuwa sekta binafsi ndio ina jukumu kubwa katika kujenga uchumi wa nchi.

 

Hali hii inaweza kuwa Baraka, na laana kwa upande mwingine.

 

Ni baraka kwa kuwa kama sekta binafsi ndio inaongoza katika kujenga uchumi wa nchi, kutatoa nafasi ya nguvu ya soko kuchagiza ubunifu na ufanisi.

 

Hali hii itaziwezesha kampuni hizo kujibu mahitaji ya walaji na shinikizo la ushindani.

 

Hata hivyo, kwa upande mwingine, serikali, kama mwanahisa mdogo, inaweza kuwa na ushawishi mdogo katika maamuzi ya kimkakati ya makampuni hizo.

 

Hii inaweza kupelekea maslahi ya umma kutowakilishwa kikamilifu katika usimamizi wa kampuni.

 

Ni kwa msingi huu, hivi karibuni Msajili wa Hazina alisema katika ulimwengu wa sasa, kukumbatia mabadiliko ya ndani ya taasisi za umma si hiari, bali ni wajibu.

 

“Mabadiliko si rahisi. Hata hivyo, hatuna budi kuyakumbatia, ili tufike kule tunakotaka kwenda,” alisisitiza Bw. Mchechu.

 

Barack Obama, Rais wa zamani wa Marekani, alisema: “Mabadiliko hayatatokea ikiwa tutangojea mtu mwingine au wakati mwingine. Sisi ndio tulio kuwa tunangojea. Sisi ndio mabadiliko tunayoyatafuta.”

 

Huu ni wito kwa watumishi wa umma kuchukua hatua ili kuchohea ubunifu na hivyo kupelekea mabadiliko katika taasisi.

 

Dhamira ya serikali katika kuleta mabadiliko si tu inalenga kuimarisha mashirika ya umma, bali pia kuhakikisha yanabaki kuwa na mwitikio kwa matarajio ya jamii.

 

Wananchi wanatarajia serikali yao sio tu kutoa huduma, bali kufanya hivyo kwa ufanisi, urahisi, na ubunifu.

 

Kadri idadi ya watu inavyokua na kuwa tofauti zaidi, taasisi za umma lazima ziendane na mabadiliko hayo ili kukidhi mahitaji mbalimbali ya wananchi wao.

 

Hii inahitaji mabadiliko kutoka mbinu za jadi kwenda kwa njia za kisasa, zinazoongozwa na teknolojia.

 

Bw. Thobias Makoba, msemaji mkuu wa serikali, alisema hivi karibuni kwamba ili mabadiliko kwenye taasisi na mashirika ya umma yaende vizuri, mawasiliano madhubuti ni lazima.

 

Alisema mawasiliano mazuri yanakuza uelewa wa pamoja kuhusu maono na malengo ya mchakato wa mabadiliko.

 

“Viongozi wanapofafanua sababu za mabadiliko na faida zinazotarajiwa, wafanyakazi wanakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kukumbatia mipango mipya ya taasisi au shirika husika,” alisisitiza Bw. Makoba, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya  Habari Maelezo.

 

Kauli hiyo inaungwa mkono na Simon Sinek, mwandishi nguli wa vitabu kutoka marekani, ambaye amewahi kusema: “Watu hawanunui kile unachofanya; wananunua kwa nini unakifanya.”

 

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Sahara Ventures, Jumanne Mtambalike, alisema hivi karibuni kwambaa mageuzi katika mashirika ya umma yanahusisha kufikiri kwa tofauti ili  kuboresha utoaji wa huduma, kuongeza ufanisi, na kukidhi mahitaji ya wananchi yanayo badilika mara kwa mara..

 

“Mabadiliko haya ni ya mfumo mzima na mara nyingi yanahusisha shirika zima----yanakusudia kubadilisha mitazamo, kuboresha uwezo, na kuwezesha athari chanya za muda mrefu,” alisisitiza.

 

Dk. Lufunyo Hussein, Mkuu wa Chuo cha Bandari, hivi karibuni alisisitiza umuhimu wa mageuzi katika taasisi za umma ili kuboresha ufanisi.

 

Alisisitiza kwamba ili kufanikiwa katika hili, mafunzo kwa watumishi wa umma ni lazima yakumbatiwe.

 

Dk. Lufunyo alisema mashirika yanapaswa kuwekeza katika mafunzo hadi asilimia 10 ya malipo yao ya mishahara, wakati wa kipindi cha mabadiliko ili kuhakikisha wafanyakazi wana ujuzi na maarifa muhimu.

 

           Makala hii imeandaliwa na

          Ofisi ya Msajili wa Hazina