Mageuzi ya Ofisi ya Msajili wa Hazina katika tathmini ya bodi
Mageuzi ya Ofisi ya Msajili wa Hazina katika tathmini ya bodi
Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Hazina imepiga hatua kubwa mbele katika kubadilisha jinsi tathmini ya bodi za Mashirika ya Umma na ya Kisheria (PSCs) zinavyofanyika.
Awali, tathimini zilifanyika kwa michakato ya mikono, ambayo mara nyingi ilikuwa polepole na isiyo na ufanisi.
Ni katika muktadha huo, Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa sasa imekumbatia suluhisho la kisasa linalolenga kuleta mapinduzi katika usimamizi wa taasisi 309 zilizo chini ya uangalizi wake.
Mabadiliko haya makubwa yamekuja kama suluhisho ya changamoto ambazo Ofisi hiyo imekuwa ikikutana nazo pindi ikiwa inafanya tathimini ya bodi za taasisi.
Njia ya jadi ilisababisha kutokamilisha tathimini kwa wakati na ufanisi.
Na kutokana na sababu hiyo, hitaji la mabadiliko halikuweza kuepukika.
Suluhisho lilikuwa wazi: kwenda kidijitali linapokuja suala la tathmini.
Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, alisema hivi karibuni kwamba ofisi yake iliamua kwenda kidijitali ili kuimarisha usimamizi wa taasisi inazozisimamia.
”Ofisi ya Msajili wa Hazina imekuwa ikifanya tathmini ya bodi ‘manually’ ambayo imekuwa na athari ya kukamilisha taasisi chache na kushindwa kuzifikia taasisi zote kwa wakati stahiki,” alisema Bw. Mchechu.
Aliendelea kueleza: “Katika kutekeleza maelekezo ya kuimarisha usimamizi wa taasisi, katika kipindi cha mwaka mmoja ofisi imefanikiwa kuanzisha ‘online board evaluation tool ‘ ambayo tayari imeanza kutumika.”
Katika kipindi hiki cha mwaka mmoja, alielezea Bw. Mchechu, Ofisi imefanya tathmini ya bodi 72 kati ya lengo la taasisi 70 ikiwa ni ufanisi wa asilimia 102.
“Kwa sasa, tunatumia nguvu ya teknolojia kuboresha tathmini za bodi, kupunguza muda unaohitajika kumaliza na kufanya mchakato kuwa wazi zaidi,” alisisitiza Bw. Mchechu.
“Njia hii ya kidijitali inafanya tathmini kwa uharaka, usahihi na ubora. Haya ni mageuzi chanya kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
“Ufanisi tulioupata katika kipindi cha mwaka mmoja tu, tukizidi lengo letu kwa asilimia 102, ni ushahidi wa wazi juu ya ufanisi wa mfumo huu.”