Mhe. Rais: Mafuru ameacha alama Mashirika ya Umma
Dar es Salaam. Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amesema mageuzi yanayoendelea kwenye mashirika ya umma ni matunda ya Marehemu Lawrence Nyasebwa Mafuru.
Mhe Rais ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa kuuaga mwili wa Bw. Mafuru, aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, kabla ya kufariki Novemba 9 katika hospitali ya Apollo, nchini india ambako alikuwa anapatiwa matibabu.
Dk. Samia alieleza kuwa mageuzi katika mashirika ya umma yaliyoanzishwa na Bw. Mafuru akiwa Msajili wa Hazina kati ya mwaka 2014 na 2016, yamekuwa na matokeo makubwa kwa Taifa.
“Mageuzi haya yanayoendelezwa vizuri na Mchechu (Nehemiah Mchechu---Msajili wa Hazina wa sasa), yalianzishwa na Lawrence,” alisema Mhe. Rais.
Mhe. Rais alienda mbali kwa kusema kuwa mwezi Julai, Mwaka jana hakumteua Bw. Mafuru kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango kwa bahati mbaya, bali ni kutokana na historia yake nzuri ya kiutendaji.
“Lawrence alikuwa ni zawadi nzuri kwa taifa letu. Lawrence ni moja ya mashujaa wa Taifa hili la Tanzania,” alisema Dk. Samia.
Aliongeza: “Akiwa sekta binafsi na hata alivyoenda sekta ya umma Lawrence alifanya kazi kwa weledi mkubwa. Kwa hakika ameacha alama isiyofutika katika Taifa hili.”
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, alimuelezea Bw. Mafuru kama mtu aliyekuwa hodari katika kazi.
“Sifa zote ambazo watu mbalimbali wamemmwagia Lawrence ni za kweli,” alisema kwa ufupi Mhe. Waziri Mkuu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo alimuelezea Bw. Mafuru kama mzalendo wa kweli.
Alisema Bw. Mafuru hata alipokuwa hospitalini nchini India bado aliendelea kutoa mchango wake kwenye utengenezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025/2050.
“Lawrence alikuwa na nidhamu ya utaalamu ya hali ya juu,” alihitimisha Prof. Mkumbo.
Kwa upande wake Bw. Mchechu, alikiri kuwa Bw. Mafuru alifanya kazi nzuri sana alipokuwa Msajili wa Hazina.
“Bw. Mafuru alitengeneza msingi mzuri katika Ofisi ya Msajili wa Hazina na ndio maana leo hii kuna mageuzi makubwa yanaendelea kufanyika katika mashirika ya umma,” alisema Bw. Mchechu.
“Somo tunalolipata kutoka kwa Mafuru ni kwamba matendo tunayo yatenda leo, yanaishi si tuu kwenye kizazi cha sasa, bali hata kizazi kijacho,” alisema Bw. Mchechu.
Bw. Mafuru ameacha mke, Bi Noela Novatus Mafuru, na watoto wawili Lorraine na Lorna Mafuru.
Habari hii imeandaliwa na
Ofisi ya Msajili wa Hazina