TISEZA yachukua nafasi ya TIC na EPZA

Na Mwandishi wa OMH
Dar es Salaam. Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Alhamisi ya Februari 13, 2025, lilipitisha Muswada wa Sheria ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.
Sheria hiyo imeanzisha Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (Tanzania Investment and Special Economic Zones Authority – TISEZA), ambayo inachukua nafasi ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Kukuza Mauzo ya Bidhaa Nje ya Nchi (EPZA), taasisi ambazo kwa sasa zimeunganishwa.
Kuunganishwa kwa taasisi hizi mbili ni sehemu ya mageuzi yanayofanywa na serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) yakiwa na lengo la koboresha utendaji kazi wa taasisi za umma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Prof Kitila Mkumbo, alisema bungeni Dodoma kuwa sheria hiyo pia imeweka mfumo wa kutoa fursa na vivutio mahsusi kwa wawekezaji wa ndani pekee, pamoja na kuanzisha Benki ya Ardhi kwa ajili ya uwekezaji.
Kupitia benki hiyo, alifafanua, mbali na ardhi itakayotengwa na TISEZA, watu binafsi na kampuni zitakuwa na nafasi ya kusajili ardhi zao na kuunganishwa na wawekezaji mbalimbali.
Ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wawekezaji, sheria imeanzisha Kituo cha Huduma Mahala Pamoja (One Stop Facilitation Centre), ambacho kitahakikisha huduma zote za taasisi mbalimbali za serikali zinazohusu uwekezaji zinapatikana kwa pamoja kidigitali.
Sheria hiyo pia inabainisha vigezo vya wawekezaji wa kimkakati kwa kuzingatia kiwango cha mtaji na vipaumbele vya kitaifa.
Kwa mujibu wa sheria, mwekezaji wa ndani anatakiwa kuwa na mtaji usiopungua Dola milioni 20 za Marekani, huku mwekezaji wa kigeni atapaswa kuwa na mtaji wa Dola milioni 50 ili kutambulika kama mwekezaji wa kimkakati.
Aidha, sheria imeweka taratibu na vigezo vya kuanzisha maeneo maalum ya kiuchumi kwa lengo la kuvutia uwekezaji zaidi.
Prof Mkumbo alisema mabadiliko hayo hayataathiri shughuli za uwekezaji zinazoendelea, bali yataimarisha mazingira rafiki ya uwekezaji nchini na kusaidia kukuza uchumi kupitia uwekezaji wa kimkakati.