Safari ya Taasisi za Umma kujiendesha kibiashara

Na Mwandishi wa OMH
Dar es Salaam. Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imedhamiria kufanya mageuzi makubwa kwenye mashirika ya umma kwa kuyafanya yajiendeshe kibiashara.
…Na dereva wa safari ya mageuzi hayo ni Ofisi ya Msajili wa Hazina chini ya Bw. Nehemiah Mchechu, ambaye ni Msajili wa Hazina.
Mashirika haya ya umma, kwa muda mrefu yamekabiliwa na changamoto za kuweka mzania sawa kati ya utoaji huduma na kutengeneza fedha kwaajili ya kujiendesha bila kuwa na utegemezi mkubwa kutoka kwa serikali kuu.
Ni Katika muktadha huo, serikali inataka hadithi hiyo ibadilike kwa taasisi hizo kubadilisha namna ya utendaji kazi wao---hivyo kuwa na ufanisi zaidi.
Akizungumza hivi karibuni mkoani Arusha, Mhe. Rais Samia alisema serikali haitavumilia mashirika ya umma ambayo yatakuwa yanajiendesha kwa hasara.
Ni katika mazingira hayo, Bw. Mchechu, ambaye ofisi yake imepewa dhamana ya kufanya mageuzi kwenye mashirika hayo, amekuwa akinukuriwa mara kadhaa akisema anataka mashirika ya umma yenye tija kwa Taifa.
“Tunataka mashirika ya umma yawe na mtazamo wa kibiashara, ili yaweze kutoa huduma bora, kuvutia wateja wengi, na hatimaye kupata faida,” alieleza Bwana Mchechu hivi karibuni.
Lengo la serikali, alieleza, sio kuingia kwenye biashara kushindana na sekta binafsi na kwamba haitasahau jukumu lake la msingi la kuwapatia watanzania huduma bora kwa gharama rafiki.
“Tunachotaka sisi ni kuona taasisi za umma zikishindana kufikiri na kufanya shughuli zao kibiashara ili zitoe huduma bora katika jamii na kupata faida itakayoziwezesha kujiendesha na kuwa na mchango mkubwa kwa Taifa,” alisisitiza Bw. Mchechu.
Kihistoria, mashirika mengi ya umma nchini Tanzania yamekuwa yakitegemea ruzuku kutoka serikalini, na hivyo kuwa mzigo kwa serikali.
Hata hivyo, mageuzi haya yana lengo la kupunguza utegemezi huu.
Kama sehemu ya mageuzi, serikali inajipanga kuhakikisha uongozi ndani ya mashirika ya umma unaimarishwa.
Bwana Mchechu alisisitiza haja ya wakurugenzi, wajumbe wa bodi, na wenyeviti wa mashirika ya umma kuwa na ujuzi wa sekta husika ili kuleta tija kwa taasisi za umma.
Wachumi waunga mkono
Mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma Dk. Lutengano Mwinuka alisema hivi karibuni kuwa kama mashirika ya umma yatajiendesha kwa muundo wa kibiashara yataweza kustawi vizuri.
“Ndio, kazi ya serikali ni kutoa huduma, lakini ili taasisi ya umma ijiendeshe huwezi ukakwepa moja kwa moja ‘elements’ za biashara,” alisema.
“Kama ilivyo kwa sekta binafsi, kwenye sekta za umma kunahitajika ufanisi, ubunifu na utoaji wa huduma bora kwa wakati.”
Ili kuwa na ufanisi mkubwa kwenye sekta za umma, Dkt Mwinuka alionesha haja ya kuwa na ubia na sekta binafsi pale inapobidi, jambo ambalo serikali inasema iko tayari kufanya hivyo.
Kwa upande wake mchumi na mtaalamu wa biashara Dk. Donath Olomi alisema hivi karibuni kuwa licha ya kwamba taasisi za umma zina jukumu la kutoa huduma, zina nafasi ya kuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi kama zitafanyiwa mageuzi makubwa ya kiutendaji.
Kwa mujibu wa takwimu rasmi za serikali, sekta ya umma inachangia asilimia 20 ya ajira zote nchini.
“Ili kuongeza mchango wa sekta ya umma kwenye uchumi wa nchi, mashirika ya umma yanapaswa kuwa na ubunifu na kutoa huduma bora kwa wakati,” alishauri Dk. Olomi.
Aliongeza kuwa ili mashirika hayo ya umma yafanye vizuri lazima wanaopewa dhamana ya kuyaongoza wawe na fikra za kibiashara.
Dk. Olomi alishauri kuwa watakaoaminiwa kuongoza mashirika hayo wapimwe kwa matokeo.
“Lazima kuwe na utaratibu wa ufuatiliaji na uwajibikaji,” alisisitiza.
Mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof. Abel Kinyondo alisema hiv karibuni kuwa taasisi za umma zikitoa huduma kwa bei nafuu, zitavutia wateja wengi na hivyo kupata faida kubwa.
Hii, alisema, itapelekea taasisi hizo kujiendesha zenyewe na kutoa gawio kubwa kwa serikali.
"Taasisi za umma kujiendesha kama za kibiashara zitaipunguzia serikali mzigo kwani zitakuwa na uwezo wa kusimama zenyewe bila msaada kutoka serikali kuu," alisema Prof. Kinyondo.
Lakini, alitoa angalizo kuwa ili hilo liwezekane inapaswa huduma zinazotolewa ziwe na ubora mkubwa, zitolewe kwa wakati, kwa ulimi mtamu na bei ambayo haitamuumiza mwananchi.
"Taasisi za umma zinapaswa kutoa huduma kwa bei nafuu ikilinganishwa na sekta binafsi. Kwa upande mwingine, taasisi hizo zinapaswa kuendesha shughuli zake kwa gharama ndogo ili zisipate hasara," alishauri Prof. Kinyondo.
Serikali imewekeza Sh86.3 trilioni katika taasisi za umma na kampuni ambazo serikali ina hisa chache 309 (kwa ujumla).
Mageuzi mapya yanayofanywa na serikali katika taasisi za umma yana lengo la kuhakikisha kuwa uwekezaji huu unakuwa na tija kubwa kwa Taifa.