TAARIFA KWA UMMA

JUMLA YA TAASISI NA MASHIRIKA YA UMMA 23 KATI YA 33 YALIYOKUWA YASAINI MIKATABA YA UTENDAJI KAZI NA SERIKALI LEO KUPITIA OFISI YA MSAJILI WA HAZINA (OTR) YAMESAINI MIKATABA YAO.

Jumla ya Taasisi na Mashirika ya Umma 23 kati ya 33 yaliyokuwa yasaini Mikataba yao ya Utendaji Kazi baina yake na Serikali, yamesaini mikataba hiyo hatua inayofungua milango zaidi kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Tano kuweza kusimamia na kukagua ufanisi wa taasisi na mashirika hayo katika kuleta tija na maendeleo ya Taifa.

Taasisi na Mashirika hayo 23 ambapo 10 kufikisha 33 yametoa udhuru wa kikazi na hivyo kuamuliwa kusaini baadae ni pamoja na; Chuo Kikuu cha Ardhi, Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Chuo Kikuu cha Dodoma, Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji, Mamlaka ya Udhibiti Bima Tanzania, Mamlaka ya Bandari Tanzania, Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha, Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania, Taasisi ya Usimamizi wa Mahakama, Chuo cha Taifa cha Usafirishaji, Hospitali ya Taifa Muhimbili, State Mining Corporation, Shule ya Sheria kwa Vitendo Tanzania, Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania, Centre For Agricultural Mechanization and Rural Technology, Bodi ya Usajili wa Wataamu wa Mipango Miji, Shirika la Elimu Kibaha, Tanzania Engineering and Manufacturing Design Organization, Taasisi ya Kansa Ocean Road na Bodi ya Nyama Tanzania.

Akitoa taarifa ya awali ya tathmini ya mikataba iliyopita ambayo itafanyiwa zoezi la kujiridhisha mapema mwezi huu wa Septembe 2017, Msajili wa Hazina Dkt.Oswald Mashindano, amesema Ofisi yake imeandaa taarifa ya awali ya tathmini ambayo imezingatia zaidi maeneo manne ambayo ni; Utendaji Kifedha, Usimamizi wa Rasilimali Watu, Huduma kwa Wateja na Utawala Bora.

Msajili wa Hazina amesema katika taarifa hiyo ya awali Ofisi imebaini yafuatayo; “Pamoja na kuwa matokeo ya jumla ya tathmini ya utendaji kazi kutoka 2014/15 hadi 2016/17 yanatoa mwelekeo mzuri wa namna Taasisi na Mashirika ya Umma yanavyotekeleza majukumu yake kwa kila mwaka wa fedha, kuna maeneo ambayo baadhi ya Taasisi zinahitaji kuyasimia ipasavyo ili yaweze kuimarika na kuboresha utendaji.”

“Asilimia 25 ya Mipango Mkakati (Strategic Plans) ya Taasisi imebainika kuwa haiendani na kazi (activities) zilizobainishwa kwenye mpango wa bajeti wa mwaka (MTEF), hivyo kuhitajika uboreshaji wa mipango mkakati husika,” amesema Dkt.Mashindano.

Ameongeza kuwa malengo yaliyobainishwa (objectives) kwenye Mpango Mkakati kwa baadhi ya Taasisi na Mashirika ya Umma haiendani na kazi (activities) zilizomo kwenye Mpango wa Bajeti unaotekelezwa (MTEF), hii ikiwa ni pamoja na maeneo ya usimamizi wa rasilimaliwatu na Utawala Bora kwa baadhi ya mashirika na taasisi za Serikali yako chini alama 10 kati ya alama 25 zilizotarajiwa ambapo usimamizi zaidi unahitajika ili kuimarisha usimamizi katika eneo husika.

Pia, Msajili wa Hazina ameweka msisitizo zaidi kuwa eneo la ukusanyaji mapato kwa baadhi ya taasisi linahitaji kuwekewa mkakati kwavile baadhi ya taasisi kwa kutumia taarifa ya awali inaonyesha alama 17 kati ya alama 25 hivyo nguvu zaidi inahitajika ili kuimarika kwa mapato ya ndani ya taasisi.

Dkt.Mashindano amesema eneo la huduma kwa wateja (Customer Service) nalo linahitaji kusimamiwa ipasavyo ikiwamo kuwa na Mkataba wa Huduma kwa Wateja (Client Service Charter), kwani mashirika mengi zaidi ya asilimia 50 yamepata alama 12 kati ya 25 zilizotarajiwa.

Katika maelezo ya jumla Msajili wa Hazina Dkt. Oswald Joseph Mashindano, amesema lengo la kuingia mikataba hiyo ni kuweka mifumo, kanuni, mikakati ya utendaji, kuboresha usimamizi wa taasisi na mashirika ya umma hapa nchini na pia ni ahadi kubaini kama malengo ya Taifa yanafikiwa kupitia taasisi na mashirika haya ambako pesa ya Serikali zinaenda ili kuhakikisha mapato na faida kwa nchi inapatikana.

Hali kadhalika katika zoezi la utiaji saini Mikataba hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) na Spika wa Bunge mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Anne Makinda, akitoa shukurani kwa niaba ya wajumbe amesema, “Mafanikio ya kila mtu ni namna anavyoweza kukabili changamoto. Naamini tukifanya kazi vizuri nchi itasonga mbele kwani mikataba tunayosaini inatupa dira ya malengo yetu ikiwa ni dhamana tuliyopewa na Rais wetu katika mchango wa maendeleo ya nchi.”

Katika maelezo ya awali Dkt.Mashindano amesema, “Ofisi ya Msajili wa Hazina mpaka sasa inasimamia Taasisi na Mashirika ya Umma yapatayo 265 yanayotoa huduma mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kusaidia katika kuchangia pato la Taifa. Aidha, Taasisi na Mashirika hayo yanatumia kiasi kikubwa cha fedha za Umma kwa njia ya mitaji, mishahara na nunuzi mbalimbali. Kwa misingi hiyo, ni vema Taasisi na Mashirika hayo yakasimamiwa ipasavyo ili yaweze kutoa huduma sahihi na endelevu na kuhakikisha kuwa, eneo la matumizi ya fedha na mali za Umma linasimamiwa ipasavyo ili kuipunguzia mzigo Serikali na kuchangia katika Mfuko Mkuu wa Serikali.

Kusainiwa kwa mikataba hii 23 kati ya 33 iliyokuwa isainiwe leo, kunafanya taasisi hizo kuwa miongoni mwa taasisi na mashirika ya awali ya umma kati ya 71 mpaka sasa yaliyoipa fursa Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) kuzikagua na kupima ufanisi wao kiutendaji kwa kila mwaka wa fedha tangu kuanza kwa zoezi hili mwaka 2014 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mujukumu yake ya kisheria kwa mujibu wa kifungu cha 10 (2) (k) cha Sheria ya Msajili Sura 370 na kama ilivyorekebishwa mwaka 2010.

Imetolewa na:

Gerard Julius Chami

Kaimu Mkuu wa Kitengo

Uhusiano, Habari na Mawasiliano,

Ofisi ya Msajili wa Hazina,

DAR ES SALAAM.

05 Septemba, 2017.