Kampeni ya uelimishaji chakula na lishe kwa watumishi wa umma serikalini yahudhuriwa kwa idadi kubwa na watumishi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Furaha Kalenga, OMH Trainee (TIA – Dsm).

Kampeni ya kutoa elimu ya chakula na lishe kwa watumishi wa umma Serikalini inayoendeshwa na Shirika la Chakula na Kituo cha Lishe Tanzania lililo chini ya Serikali (TFNC), imefanyika kwa mafanikio makubwa baada ya zaidi ya theluthi mbili ya watumishi wote wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) kuhudhuria warsha ya kampeni hiyo iliyofanyika jijini Dar Es Salaam katika Ukumbi wa Ruaha wa Kituo cha Kimataifa wa Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC).

Akielimisha watumishi wa OTR zaidi ya 76 waliohudhuria warsha hiyo, mwezeshaji wa warsha hiyo kutoka Shirika la Chakula na Kituo cha Lishe Tanzania lililo chini ya Serikali (TFNC), Ndugu Benard Makene amesema, “Dhumuni la warsha hii ni kukumbushana hali kdhalika kutoa elimu kwa kila mtumishi kujali afya kwa kula mlo kamili kama sehemu ya ulaji unaofaa ili kuondokana na asilimia 70 za magonjwa yasiyoambukizwa.”

Ndugu Benard Makene ameongeza kuwa lengo jingine kubwa linalotiliwa mkazo na nguvu zaidi katika kupunguza matatizo ya chakula na lishe kwa watumishi wa umma ni kuipunguzia Serikali gharama kubwa za kusaidia wananchi na hasa watumishi wa umma wenye matatizo sugu kama yale ya; figo, moyo na mengineyo hatarishi ambayo yanaweza kuepukika na kuepusha gharama kubwa kwa Serikali kuyagharamia na badala yake fedha hiyo kutumika katika shughuli nyingine za maendeleo kama kukarabati, kutengeneza na kuendeleza miundo-mbinu katika Taifa letu.

Ametia msisitizo kwa watumishi wa umma na familia zao kuyajua vizuri nakwa ustadi mkubwa makundi matano ya chakula na namna ya kuyatumia yakiwemo yale ya vyakula vya nafaka na mizizi vinavyoongeza madini mwilini, vyakula vya protini kama nyama,ndizi na samaki, kundi la tatu likiwa ni matunda, la nne ni mboga za majani na lile la mwisho lenye vitu vya sukari.

Akiongezea katika yaliyozungumzwa na mwasilishaji wa mada, mwezeshaji mwenza kutoka Shirika la Chakula na Kituo cha Lishe Tanzania lililo chini ya Serikali, Ndugu Aveline Munuo, ameeleza bayana kuwa endapo kila mtu atafuata mlo kamili ambao umegawanyika katika makundi hayo matano itasaidia kupunguza kasi ya magonjwa hatarishi katika Taifa letu na hivyo kuimarisha nguvu kazi ya Taifa letu.

Aidha katika majadiliano washiriki wamependekeza TFNC kufanya utafiti zaidi kwenye masuala ya chakula na lishe kupata ukweli wa yale yanayozungumzwa sehemu mbalimbali likiwemo lile la wanaume kutumia samaki kama Pweza, mihogo mibichi na karanga mbichi kama sehemu ya kuongeza nguvu za kiume ili wananchi wapate uhakika pale wanapotumia kama ni salama ili kuepusha magonjwa mengine yanayoweza kusababishwa na kuzidishwa kwa matumizi ya vyakula hivyo kwa nia hiyo.

TFNC ina jukumu la kuongeza viboresho vya kufanyia utafiti juu ya magonjwa mbalimbali na vitendea kazi kiujumla ili kupunguza tatizo la magonjwa ya kujitafutia kwa asilimia 70.

*****16082017*****