Ofisi ya Msajili wa hazina yaainisha utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa sheria ya Msajili wa Hazina.

Gerard Chami, OMH – Dsm.

Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), leo imeendelea kuainisha wajibu na majukumu yake katika usimamizi wa taasisi na mashirika ya umma yaliyo chini yake wakati wa kikao kazi wa siku moja kuhamasisha Sheria ya Msajili wa Hazina uliofanyika jijini Dar Es Salaam katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Julius Nyerere (JNICC).

Akizungumza na wajumbe zaidi ya 70 wa kikao kazi hicho ambao ni watendaji wakuu wa taasisi na mashirika ya umma, wenyeviti wa bodi za wakurugenzi wa taasisi na mashirika hayo na makatibu wakuu wa wizara mama za taasisi na mashirika hayo, Msajili wa Hazina, Dkt.Oswald Mashindano amesema, dhumu ni hasa la kikao kazi hicho ni kukumbushana wajibu na majukumu kwa mujibu wa sheria anazotumia Msajili wa Hazina ili kuwa na uelewa wa pamoja na kuondoa kupishana katika utekelezaji mara kunapokua na maelekezo yanayotakiwa kufanyiwa kazi.

Dkt. Mashindano amesema ni vema kila upande ukajua ukomo wa mipaka yake katika utekelezaji wa majukumu kwani mafanikio yoyote yanahitaji kwenda pamoja kukiwa na uelewano wa pamoja katika taratibu, kanuni na sheria zinazotuongoza na hivyo kuleta tija na maendeleo katika Taifa linaloelekea katika uchumi wa kati na uboreshaji wa viwanda.

Amefafanua kuwa endapo hili litazingatiwa basi ni wazi hakutakua na taasisi au shirika la umma litakalofanya kazi kwa hasara na badala yake ushirikiano huo utaleteleza taasisi na mashirika haya kutengeneza faida wakati wote na hivyo kuwa na uwezo mkubwa wa kuchangia katika mfuko mkuu wa pato la Serikali.

Aidha katika majadiliano baada ya uwasilishaji wa mada muhimu za kikao kazi hicho, wajumbe wamependekeza na kushauri uwepo wa ushiriki wa wadau wakati wa marekebisho yoyote ya Sheria ya Msajili wa Hazina kwani Sheria zote duniani hutegemeana wakirejelea zile zilizoanzisha taasisi na mashirika hayo ya umma na ile ya Msajili wa Hazina.

Ofisi ya Msajili wa Hazina ina jukumu la kusimamia rasilimali za Serikali ikiwemo uwekezaji wa Serikali katika Mashirika ya Umma na Kampuni binafsi. Hivyo, husimamia utendaji wa mashirika na taasisi za umma na kutoa ushauri kwa Serikali wa namna ya kuimarisha uendeshaji wa taasisi, mashirika ya umma na kampuni zipatazo 265 kwa idadi ya mpaka Desemba 2016 ikiwemo usimamizi wa mali za Serikali ambazo zilibinafsishwa zinazojumuisha viwanda 153 na mashamba 184.

Jumla ya taasisi na mashirika 36 yalishiriki katika awamu hii ya kwanza.

*****28072017*****