JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

 OFISI YA MSAJILI WA HAZINA

Anuani ya simu: “Msajili wa Hazina”

Dar Es Salaam

Simu Nambari: +255-222-121-334

Nukushi: +255-222-110-046

Barua pepe: Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Jengo la CHC zamani,

33 Mtaa wa Samora Machel,

50 Mtaa wa Mirambo,

Sanduku la Barua 3193,

11104 DAR ES SALAAM.

TAARIFA KWA UMMA

MSAJILI WA HAZINA KUTOA ‘NO OBJECTION’ KWA MAMLAKA YA USAFIRI WA ANGA (TCAA) KWA AJILI YA UNUNUZI WA RADA ZA KUONGOZEA NDEGE KATIKA ANGA LA TANZANIA NA SEHEMU JIRANI.

Msajili wa Hazina, Ndg.Lawrence Mafuru ameahidi kutoa kwa haraka sana waraka wa ‘No Objection’ kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Anga (TCAA) ili kuruhusu zoezi la kupata fedha za mkopo kutoka Benki ya Uwekezaji nchini (TIB) kwa ajili ya ununuzi wa rada 4 zitakazofungwa katika maeneo manne nchini; Dar Es Salaam, Mwanza, Songwe na Kilimanjaro zitakazokidhi kuhudumia anga lote la Tanzania na sehemu jirani na hivyo kuleteleza kuongezeka kwa mapato ya Serikali kutokana na kulifikia eneo kubwa la nchi na maeneo jirani ambapo kwa sasa sehemu ya maeneo hayo yanapatiwa huduma hizi na nchi jirani ya Kenya.

Haya yamesemwa leo wakati wa ziara ya kikazi ya Msajili wa Hazina katika Mamlaka ya  hiyo kwa lengo la kuangalia utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo na kujifunza mambo na shughuli mbalimbali zinazofanyika na kutekelezwa na TCAA ambayo ina wajibu wa kusimamia sekta ya usafiri wa anga nchini.

“Honestly, hakuna aliyeyajua haya yote yakoje kama mlivyonifafanulia na timu yangu hapa kwa maneno na vielelezo, kwakweli niko na Kaimu Mkurugenzi wa Uwekezaji hapa ambaye ndiye anashughulikia haya yote mnayoyasema hapa, anasikia, ninawaahidi waraka wa ‘no objection’ utatoka wiki hii kuja kwenu ili muendelee na zoezi linalofuata msije mkasema Msajili wa Hazina alikwamisha mchakato wetu kwa kutotupatia ‘no objection’ kwa wakati,” amesema Mafuru.

Msajili amesema ameshawishika kuunga mkono mradi wa rada wa TCAA baada ya kueleweshwa kuhusu umuhimu wake katika kukuza sekta. Pamoja na hilo ameukumbusha uongozi wa TCAA kufanya matumizi fasaha ya fedha zote zinazotengenezwa na mashirika ya Umma kama mojawapo la mashirika hayo kwani taasisi hizi ni mali ya Umma na siyo vinginevyo,  hivyo Serikali imejipanga kufuatilia kwa karibu matumizi ya fedha hizo kupitia  njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kamati za bunge ambazo zitakwua zikifuatilia kwa karibu.

Ameongez na kusisitiza kuwa, Serikali ya awamu ya tano inataka kuona mashirika ya Umma yakijiendesha kwa ufanisi pamoja na kuchangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa nchi yetu, “Serikali imebadilika kwa jinsi ambavyo inasimamia taasisi zake, huko nyuma pengine zilikuwa zinaendesha shughuli zake bila kutoa mchango mkubwa, lakini hivi sasa ni muda na awamu ya kuhakikisha mnachangia vya kutosha katika mfuko mkuu wa Serikali” amesema Mafuru.

Aidha, ametumia fursa ya ziara hiyo kuelezea azma ya Serikali katika kukuza sekta ya  usafiri  hapa nchini na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza katika sekta hiyo barani Afrika na hivyo kuelekeza TCAA kujipanga kikamilifu zaidi katika kufanikisha azma hii ya Serikali katika kukuza sekta ya usafiri wa Anga kwa sehemu yake, kwani ni jukumu la kila taasisi ya Umma kuona ni kwa jinsi gani inafikia azma ya Serikali ya  kuleta maendeleo nchini.

Ameipongeza TCAA kwa kufanya kazi kwa weledi ambapo amesema hatua hiyo imewezesha Mamlaka kutunukiwa tuzo ya utoaji wa huduma zake kwa ubora iliyotolewa hivi karibuni nchini Italia pamoja na kufanikiwa kutetea nafasi yake ya uwakilishi katika Baraza la Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga Duniani - ICAO. Msajili amesema hatua hizo zote zisingefikiwa kama Mamlaka ingekuwa Shirika lisilo na weledi.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2015/2016 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Ndg.Hamza Johari ametaja sehemu ya mafanikio yaliyopatikana ikiwemo; kuongezeka kwa mapato kutoka shilingi bilioni 52 hadi kufikia bilioni 56.2 sawa na 91.1% ya shilingi bilioni 63.2 waliyojipangia yaliyoleteleza kuchangia jumla ya shilingi bilioni 5.14 za kitanzania katika mfuko mkuu wa Serikali, kupungua kwa matukio na ajali za anga kutoka 6 hadi 5, ongezeko la idadi ya nchi zilizoingia mikataba ya usafiri wa anga na Tanzania kutoka 53/2015 hadi 61/2016, kuongezeka kwa idadi ya wasafiri wa anga wanaokuja au kupita Tanzania kutoka 4,895,833/2015 hadi kufikia 5,065,184/2016 ambalo ni ongezeka la 3.5%, safari za ndani ya nchi ziliongezeka kutoka 175,725/2015 hadi 249,011/2016 ambalo ni ongezeko la 41.7% lililotokana na ukarabati wa viwanja vya ndege na ongezeko la njia.

Akihitimisha taarifa hiyo Johari amesema, miradi mbalimbali inayotekelezwa na TCAA kwasasa ni pamoja na; mradi mkubwa wa kununua rada 4 kwa ajili ya kuimarisha huduma za uongozaji ndege na hivyo kuimarisha usalama wa anga la Tanzania pamoja na maeneo jirani yatakayofikia na rada hizo pamoja na kuongeza mapato yatokanayo na huduma za kuongezeka kwa ndege kutoka nchi na mashirika mbalimbali duniani, uwekaji wa mfumo wa kuandaa hati za madai kwa ndege zilizofanya safari katika anga la Tanzania, uwekaji na utumiaji wa mitambo ya kisasa ya kutuma na kupokea taarifa muhimu za usafiri wa anga, na usimikaji wa mitambo ya kuboresha Mtandao wa mawasiliano ya simu.

Katika ziara hiyo msajili amekutana na kuzungumza  menejimenti ya TCAA pamoja na kutembelea kituo kikuu cha kuongozea ndege kilichopo uwanja wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere (JNIA) ambapo ameona jinsi wataalam wa  uongozaji ndege wanavyotekeleza majukumu yao kwa weledi na ufasaha mkubwa kulingana na vifaa na vitendea kazi vilivyopo.

Imetolewa na:

Gerard Julius Chami

Kaimu Mkuu wa Kitengo

Uhusiano, Habari na Mawasiliano,

Ofisi ya Msajili wa Hazina,

DAR ES SALAAM.

12 Oktoba, 2016.