TAARIFA KWA UMMA

BODI ZA TAASISI NA MASHIRIKA YA UMMA 17 ZAONGEZEWA UWEZO NA MSAJILI WA HAZINA KATIKA USIMAMIZI WA TAASISI NA MASHIRIKA YA UMMA.

Jumla ya Taasisi na Mashirika ya Umma 17 yenye takribani jumla ya watendaji wakuu, wenyeviti na wajumbe wa bodi wapatao 200, yamepatiwa mafunzo ya siku moja kuhusiana na wajibu na majukumu yao katika usimamizi wa Taasisi na Mashirika ya Umma hapa nchini hasa yale yanayosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Akizungumza katika uzinduzi wa warsha hii iliyoendeshwa jijini Dodoma katika Ofisi za Hazina, Msajili wa Hazina (TR) Ndg.Athumani Selemani Mbuttuka, amesema hii ni sehemu ya watendaji wakuu, wenyeviti na wajumbe wa bodi wapya ambao wanateuliwa kila mamlaka za uteuzi zinapobaini uhitaji wa kufanya teuzi hizo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kustaafu kwa mujibu wa sheria, kuondolewa madarakani kutokana na kutokidhi vigezo au kufikia malengo kusudiwa na Serikali au kwisha kwa muda wa utumishi wa bodi hizo na hivyo kuhitajika kwa uteuzi wa bodi mpya.

Ndg.Mbuttuka akitanabaisha lengo mahususi la warsha hiyo kuwa ni kuwajengea uwezo ili kuimarisha utendaji na usimamizi wa majukumu ya Taasisi na Mashirika ya Umma kwa mujibu wa Vifungu Na.10 (2) (e) na 10 (5) vya Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370, amewapongeza wote walioteliwa kwa kusisitiza kwamba hiyo ni ishara tosha kuwa mamlaka za uteuzi zimewaamini na zinatarajia utendaji uliotukuka kutoka kwao.

Msajili wa Hazina akiwasihi wenyeviti na wajumbe wa bodi kuwa makini na wabunifu katika kufanya maamuzi sahihi kwa wakati, amewataka kuwa na mikakati madhubuti ya kukusanya mapato ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi huku wakizingatia nia njema ya Serikali katika kupunguza gharama za uendeshaji zinazotokana na matumizi yasiyo ya lazima hususani safari za bodi na viongozi zisizokua na tija kwa ofisi na Serikali kwa ujumla wake.

Hali kadhalika amewasihi sana wajumbe wa bodi kujizuia na migongano ya kimaslahi katika kusimamia utekelezaji wa majukumu ya usimamizi wa Taasisi na Mashirika hayo ikiwa ni pamoja na zuio la malipo ya posho za nyumba, simu, usafiri, maji na umeme kwa watumishi wasio na sifa za stahili hizo tofauti na ielekezavyo miongozo ya utumishi, waraka za msajili wa hazina na mamlaka nyingine zenye jukumu la kutoa miongozo hii ikiwa ni sehemu ya kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi na Utumishi wa Umma.

Pamoja na hilo Ndg.Mbuttuka ametoa maelekezo mahususi kwa kuwataka watendaji wakuu, wenyeviti na wajumbe wa bodi ambao taasisi na mashirika yao bado yanalipa watumishi viinua mgongo kusitisha mara moja malipo hayo kwa watumishi ilhali watumishi hao wakichangiwa katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwani utaratibu huu ni kinyume na Sheria za Mafao.

Aidha, kwa mara nyingine amezitaka taasisi na mashirika yote yanayopaswa kuchangia asilimia 15 ya mapato ghafi katika Mfuko Mkuu wa Serikali wanafanya hivyo kwa mujibu wa Sheria baada ya Bodi kuhakikisha na kujiridhisha kuwa mchango unaowasilishwa uko sahihi, ni halisi na unaendana na kiwango cha mapato ghafi tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo Msajili wa Hazina anawajibika kufuatilia na kujiridhisha katika hili jambo linaloongeza gharama kwa Serikali wakati Bodi zinazowajibika zipo.

Akimalizia Msajili wa Hazina Ndg.Mbuttuka amezisisitiza tena Taasisi na Mashirika ya Umma ambayo bado hayajasaini mikataba ya utendaji kazi na Msajili wa Hazina kufanya hivyo mara moja kwa mujibu wa Sheria ya Msajili wa Hazina, Kifungu cha 10 (2) (K) na rejeo la maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli wakati wa dhifa ya utoaji gawio kwa Serikali kwani taasisi na mashirika ya umma yatakayobainika kuwa na utendaji usioridhisha nay ale yanayopata hasara kila mwaka watawajibishwa kutokana na kukosekana kwa ubunifu na kutoweka mikakati ya kuboresha utendaji wao.

Taasisi na Mashirika ya Umma yaliyoshiriki awamu hii ya kujengeana uwezo ni pamoja na; Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini (GPSA), Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Tume ya Ushindani (FCC), Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), Mamlaka ya Rufaa za Ununuzi wa Umma (PPAA), Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO), Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Taasisi ya Ustawi wa Jamii (ISW), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Benki ya Maendeleo TIB (TIB DEV. BANK), Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA) na Mfuko wa Misitu Tanzania (TAFF).

Imetolewa na:

Gerard Julius Chami

Mkuu wa Kitengo

Uhusiano, Habari na Mawasiliano,

Ofisi ya Msajili wa Hazina,

DODOMA.

02 Novemba, 2018.