TAARIFA KWA UMMA

TAASISI NA MASHIRIKA YA UMMA YAPEWA MWEZI MMOJA KUHAKIKISHA YAMESAINI MIKATABA YA UTENDAJI KAZI NA SERIKALI.

SERIKALI kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imetoa kipindi cha mwezi mmoja kwa Taasisi na Mashirika ya Umma ambayo taratibu za uwekaji saini bado hazijakamilika kuhakikisha zinakamilisha na zinawekeana saini na Serikali haraka iwezekanavyo ya Mikataba ya Utendaji Kazi kwa mwaka 2018/19 kama waraka wa Katibu Mkuu Kiongozi wa mwaka 2018 unavyoelekeza.

Akizungumza katika hafla ya uwekaji saini wa mikataba ya utendaji kazi kwa Taasisi na Mashrika ya Umma 80 kwa mwaka 2018/19 leo Jumanne (Oktoba 2, 2018) Jijini Dar es Salaam, Msajili wa Hazina Ndg.Athumani Selemani Mbuttuka alisema mikataba hiyo ya kazi ni utekelezaji wa Sheria na Serikali itaendelea kusimamia Taasisi na Mashirika yao ili yaweze kufikia malengo yaliyowekwa.

Alisema kuwa katika kipindi cha miaka minne, Ofisi ya Msajili wa Hazina imefanikiwa kuingia mikataba ya utendaji kazi na Taasisi na Mashirika ya Umma 105: mwaka 2014/15 taasisi 11; mwaka 2015/16 taasisi 13; mwaka 2016/17 taasisi 28, mwaka 2017/18 taasisi 53 na kuzitaka taasisi nyingine zilizobaki kukamilisha taratibu hizo kabla Serikali haijaanza kuzichukulia hatua kwa mujibu wa Sheria.

Akifafanua zaidi alisema Ofisi yake imesajili jumla ya Taasisi na Mashirika ya Umma 185 kati ya makampuni, mashirika, wakala na taasisi 233 zilizopo nchini ambazo baadhi yake zimeunganishwa na Serikali kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika utoaji huduma kwa umma.

Mbuttuka alisema mikataba hiyo imelenga katika kuhakikisha kuwa Serikali na mashirika yanawekeana dira na malengo ili kuwa na mwelekeo unaowiana ili kuongeza ufanisi katika maeneo makuu manne ikiwemo Utawala Bora; Rasilimali Fedha; Mikataba ya Huduma kwa Wateja; na Uzingatiaji wa Kanuni, Sheria na Taratibu.

“Tumewekeana mikataba na Wenyeviti wa Bodi wa Taasisi na Mashirika ya Umma katika kuhakikisha kuwa yanaongeza tija na ufanisi zaidi ili kuleta matokeo chanya katika maeneo ya kazi na pia kuwaweka karibu zaidi na Menejimenti kuweza kufahamu kwa kina wajibu na majukumu yao katika taasisi hizo” alisema Mbuttuka.

Aidha alisema katika mikataba hiyo, Serikali imeweka mkazo zaidi katika maeneo hayo manne kwa kutambua kuwa ni sehemu muhimu zilizohitajika kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha utoaji huduma na kufanya taasisi na mashirika ya umma kuweza kujiendesha vyema na kuleta tija kwa Serikali na Umma kwa ujumla wake.

“Katika hili eneo la rasilimali watu tumeangalia zaidi mafunzo; muundo na motisha kwa watumishi maeneo ambayo yanawezesha watumishi kutekeleza vyema majukumu yao likijumuishwa kwa pamoja na eneo la usimamizi fedha ambalo nalo tumeliangalia ni kwa namna gani tutaweza kupunguza gharama zisizo za lazima katika taasisi na mashirika haya” alisema Msajili wa Hazina.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt.Khatibu Malimi Kazungu alisema Serikali imewekeana mikataba hiyo ili kubaini changamoto zilizopo katika Taasisi na Mashirika ya Umma ili kuhakikisha kuwa yanafanya kazi zake kwa kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni zilizopo katika kuleta tija na malengo yaliyokusudiwa na Serikali.

Dkt.Kazungu alisema katika utafiti uliofanyika ulibaini kuwa Taasisi na Mashirika mengi ya umma hayakuwa yakizingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za matumizi ya fedha za umma ikiwemo malipo ya posho zisizo za lazima, hivyo kupitia mikataba hiyo, Serikali itaangalia namna bora zaidi ya kuhakikisha kuwa fedha za umma zinatumika katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Cha Ushirika Moshi (MUCO), Ndg.George Yambesi alisema mikataba hiyo ya kazi itaziwezesha taasisi na mashirika ya umma kutekeleza vyema majukumu yake vile kwa kipindi kirefu Serikali imekuwa ikihitaji mikataba hiyo ili kuyawezesha kufanya kazi kwa ufanisi na kuongeza tija iliyokusudiwa.

Kusainiwa kwa mikataba hii 80 ambayo ndilo lengo kwa mwaka 2018/19, kunafanya taasisi na mashirika ya umma hayo kuwa miongoni mwa taasisi na mashirika ya awali ya umma 105 kati ya 185 yaliyosajiliwa kutoka 233 yanayosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) ambayo sasa yanafikia 185 yanayoipa fursa Serikali kupitia OTR kuzikagua na kupima ufanisi wao kiutendaji kwa kila mwaka wa fedha tangu kuanza kwa zoezi hili mwaka 2014 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mujukumu yake ya kisheria kwa mujibu wa kifungu cha 10 (2) (k) cha Sheria ya Msajili Sura 370 na kama ilivyorekebishwa mwaka 2010.

Imetolewa na:

Gerard Julius Chami

Mkuu wa Kitengo

Uhusiano, Habari na Mawasiliano,

Ofisi ya Msajili wa Hazina,

DAR ES SALAAM.

02 Oktoba, 2018.