TAARIFA KWA UMMA

WAWEKEZAJI WENYE NIA YA KUWEKEZA KATIKA VIWANDA VYA NYAMA NA NGOZI WAJITOKEZA - MSAJILI WA HAZINA.

Msajili wa Hazina, Ndg.Athumani Selemeni Mbuttuka amemthibitishia Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Luhaga Joelson Mpina (Mb) kuwepo kwa wawekezaji waliojitokeza wakiwa na nia ya kuwekeza katika viwanda vya nyama na ngozi vilivyopo mkoani Shinyanga, Mwanza na Mbeya ambavyo vilibinafsishwa miaka ya nyuma na Serikali kubaini vinafanya kazi kwa kusuasua na vingine kufa kabisa.

Amethibitisha hili wakati wa ziara fupi na kikao kazi na Waziri Mpina kilichofanyika hii leo katika ukumbi mdogo wa mikutano uliopo katika Ofisi ya Msajili wa Hazina Mtaa wa Mirambo 50 jijini Dar Es salaam.

Akimthibitishia hilo Mheshimiwa Waziri, Msajili wa Hazina amesema, “Wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika viwanda vya nyama na ngozi mkoani Shinyanga, Mwanza na Mbeya wamejitokeza na kuonyesha nia yao hiyo waziwazi, hivyo hatua iliyopo sasa ni kuambatana na wawekezaji hao tuwapeleke wakaone na kukagua sehemu husika ya kiwanda anachohitaji kufanya uwekezaji wake baada ya zoezi la ukaguzi na tathmini ya mali iliyopo kukamilika.”

Aidha, Waziri Mpina pamoja na pongezi alizotoa kwa Ndugu Mbuttuka kuteuliwa kuwa Msajili wa Hazina na jitihada zilizofanywa na Ofisi ya Msajili wa Hazina mpaka kufanikisha Wakala, Kampuni, Taasisi na Mashirika ya Umma kutoa gawio kwa mwaka wa Fedha 2017/ 2018; amesisitiza kuwa jukumu la Ofisi hii ni kubwa sana ikiwemo kubaini changamoto za uwekezaji wa Serikali na kuweza kuishauri Serikali namna bora ya kuzishughulikia changamoto hizo ili iweze kunufaika na uwekezaji wake na kuleta tija kwa Taifa.

“Naomba kama mlivyopewa majukumu haya na Serikali ni vema eneo hili la usimamizi na uangalizi likatazamwa kwa jicho la pekee na kupewa nguvu zote kwani ukaguzi, ufuatiliaji na tathmini ni muhimu sana na ndiyo maana pia naungana nanyi katika hoja yenu ya kutaka kuongezewa nguvu kazi zaidi yenye weledi na sifa stahiki ili kukidhi hitaji hili na tufikie adhma ya Serikali yetu.” Amesema Waziri.

Waziri Mpina ameongeza kuwa kufufuliwa na kuweza kufanya kazi vema kwa viwanda vya sekta hii ya mifugo kutawezesha kupunguza au kuondoa kabisa janga la utoroshwaji wa wanyama wetu kama ng’ombe ambapo ng’ombe milioni 1.6 hutoroshwa kila mwaka hapa nchini na katika kipindi cha miezi mitatu mpaka sasa jumla ya ng’ombe 37,000 na mbuzi 125,000 wamekamatwa sehemu mbalimbali hasa katika mipaka yetu wakitoroshwa.

Akihitimisha Mheshimiwa Waziri Mpina amesema, katika nchi yoyote duniani Serikali hupimwa kwa utekelezaji wake katika kipindi itakachokaa madarakani, hivyo ni vema kuongeza nguvu na kasi ya utekelezaji wa majukumu ya msingi yaliyokasimiwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina ili kufikia malengo ya Mpango wa Miaka mitano, Ilani ya Chama Tawala na malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli.

Nae Msajili wa Hazina amemalizia kwa kuwasilisha ombi kwa Mheshimiwa Waziri la kuitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu zaidi kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina katika utekelezaji wa majukumu yake pamoja na maagizo na maelekezo inayotoa kwa Taasisi na Mashirika ya Umma yaliyo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Imetolewa na:

Gerard Julius Chami

Mkuu wa Kitengo

Uhusiano, Habari na Mawasiliano,

Ofisi ya Msajili wa Hazina,

DAR ES SALAAM.

10 Agosti, 2018.